(Swahili) Ni jambo gani linaloweza kuwa baya kuhusiana na upandaji miti? Shinikizo jipya kuhusu upandaji wa miti kwa ajili ya viwanda Kusini mwa Dunia

Katika kijitabu hiki, WRM inalenga kuvitahadharisha vikundi vya wanajamii na wanaharakati kuhusu msukumo mpya wa makampuni unaolenga kukuza na kupanua upandaji wa miti ya kibiashara ya aina moja. Kijitabu hiki pia kinauweka bayana ukweli wa ubaya wa upandaji miti ya aina moja katika kiwango kikubwa na madhara yake, na ukweli huu unazungumziwa bila kujali mbinu zao za kunadi soko lao, hasa kwa kutumia kauli inayo onyesha kuwa upandaji miti utakuwa ni “suluhisho” la majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabia-nchi.

>>> Pakua chapisho katika pdf

Ni jambo gani linaweza kuwa baya kuhusiana na upandaji miti? Je, wanajamii ulimwenguni si wamekuwa wakipanda aina mbalimbali za miti tangu enzi za ustaarabu wa binadamu?

Ndio, wanajamii wamekuwa wakipanda hiyo miti mbalimbali. Lakini katika nyakati za hivi karibuni, makampuni yamekuwa pia yakipanda miti, hasa katika mabara ya Afrika, Asia, na Amerika ya Kusini, lakini namna wanavyopanda miti ni tofauti na namna wanajamii wanavyofanya. Makampuni haya hupanda maeneo makubwa kwa miti ya aina moja, huku wakitengeneza mashamba makubwa ya miti ya aina moja ambayo hayasaidii bayoanuai.

Hivi sasa, makampuni haya haya yanapanga kuanzisha upanuzi mpya mkubwa wa mashamba ya miti.Wanatumia mwanya wa ufahamu na hofu kubwa ya umma kuhusu mabadiliko ya tabia-nchi, makampuni hayo yanadai kuwa upandaji wa miti ya aina moja ni njia bora kabisa ya kusaidia matatizo yanayoukabili ulimwengu hivi sasa: kupotea kwa misitu, kuongezeka kwa joto duniani na kutegemea zaidi mafuta yatokanayo na visukuku yaani mafuta ya dizeli na petroli, makaa ya mawe, na gesi asilia.

Hoja ya makampuni ni kwamba upandaji wa miti ya aina moja utahamasisha “urejeshaji wa misitu”, na upandaji huo wa miti unaweza kuwa “suluhisho” la kiasili kwa changamoto za mabadiliko ya tabia-nchi, na kwamba upandaji huo utasaidia kukuza “uchumi wa kibailojia”. Hata hivyo, ukweli halisi ni kuwa viwanda vinavyohusika vinahitaji mashamba mengi zaidi ya miti ya aina moja ili kuongeza wigo wao wa faida. Viwanda vingine na wachafuzi wa hewa wengine wanatumia mbinu za uongo na ulaghai kama hizo kwa lengo la kuficha mchango wao katika majanga ya kijamii na kimazingira kwa sayari yetu.

Katika kijitabu hiki, WRM inalenga kuvitahadharisha vikundi vya wanajamii na wanaharakati kuhusu msukumo mpya wa makampuni unaolenga kukuza na kupanua upandaji wa miti ya kibiashara ya aina moja. Kijitabu hiki pia kinauweka bayana ukweli wa ubaya wa upandaji miti ya aina moja katika kiwango kikubwa na madhara yake, na ukweli huu unazungumziwa bila kujali mbinu zao za kunadi soko lao, hasa kwa kutumia kauli inayo onyesha kuwa upandaji miti utakuwa ni “suluhisho” la majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabia-nchi.

Moja kati ya mafunzo tuliyojifunza toka katika mapambano ya kuzuia upandaji wa miti kwa ajili ya viwanda duniani katika miaka ya hivi karibuni: ni bora kabisa kuzuia upandaji wa miti kabla haujaanzishwa rasmi, kuliko kujaribu kuzuia upandaji wa miti wakati miti imeshapandwa kwenye ardhi.

Huu ni wakati muhimu sana wa kuimarisha vikundi vya kijamii, ni wakati wa kuunganisha nguvu na kuchukua hatua za kivitendo za moja kwa moja ili kukomesha mipango ya upanuzi wa mashamba ya miti ya aina moja kwa matumizi ya viwandani mapema. Vinginevyo, hata ardhi ya jamii itapotea na njia za kujikimu za wakulima wadogo zitaharibiwa.

Ili kuanzisha majadiliano na mashauriano kuhusu matatizo yahusianayo na upandaji miti ya kiviwanda, kijitabu hiki kinatoa maswali ambayo yameshauriwa mwishoni mwa kila kipengele. Maelezo yaliyotolewa katika sehemu mbalimbali za kijitabu hiki yametoka katika vyanzo mbalimbali vya taarifa, na pia mwisho wa kijitabu hiki kuna mapendekezo yametolewa kwa ajili ya kujisomea zaidi.

>>> Pakua chapisho katika pdf