(Swahili) Tanzania: Upinzani wa wanajamii dhidi ya mashamba makubwa ya miti

Kwa mtazamo wa mara ya kwanza, kijiji cha Nzivi kinafanana na vijiji vingine katika eneo lile. Lakini kijiji hicho kina tofauti kubwa na vijiji vingine kwa sababu hakiruhusu wawekezaji wanaotaka kupanda mashamba makubwa kama vile upandaji wa mashamba makubwa ya miti. Kampuni ya Green Resources ni kampuni kubwa zaidi inayojihusisha na upandaji wa mashamba ya miti nchini Tanzania.

Kwa mtazamo wa mara ya kwanza, kijiji cha Nzivi, kilichopo katika mkoa wa Iringa nchini Tanzania, kinafanana sana na vijiji vingine vingi katika eneo lile. Wakazi wake wanaishi kwa kutegemea shughuli za kilimo na ufugaji wa ng’ombe, na hizo ndizo kazi kuu wanazozifanya wananchi wa kijiji hiki. Lakini mtu yeyote atakaye kitembelea kijiji hiki atashangazwa na mashamba makubwa ya miti yaliyokizunguka kijiji hicho, mashamba hayo makubwa ya miti ni yale ya miti ya paina na mikaratusi. Kwa ujumla wake, inawezekana ikawa ndio mashamba makubwa zaidi ya miti katika nchi za Afrika ya Mashariki. Hadi kufikia mwaka 2016, Tanzania ilikuwa na takribani hekta laki 583 zilizokuwa zimepandwa miti, kati ya hizo hekta zaidi ya laki 400, ambazo ni wastani wa asilimia 70 zinapatikana katika mikoa ya Iringa na Njombe, eneo linalojulikana kama Nyanda za Juu Kusini.

Lakini mtu yeyote atakaye zungumza na wanajamii wa kijiji cha Nzivi atagundua kuwa wananchi wa kijiji hicho wapo tofauti ukilinganisha na vijiji vingine kwa kuzingatia mambo makuu mawili: baada ya kuwa wamejifunza kutokana na uzoefu wa vijiji vingine, waliamua kutoruhusu wawekezaji wakubwa ikiwemo uwekezaji wa mashamba makubwa ya miti. Na kutokana na uamuzi huo, kijiji cha Nzivi bado kina eneo kubwa la ardhi linalotumika kwa mahitaji ya msingi ya wanakijiji wote.

Ili kufahamu sababu zilizowafanya wanakijiji wa Nzivi kufanya maamuzi hayo, ni vema kufahamu athari za mashamba makubwa ya miti kwa ajili ya viwanda kwa jamii zingine katika eneo lile. Mwaka 2018, mashirika ya kiraia ya SUHODE Foundation, Justiça Ambiental na WRM yalitembelea vijiji mbalimbali. Pamoja na kukitembelea kijjiji cha Nzivi, yalitembelea pia vijiji vya Idete, Mapanda, Kihanga, Igowole na Taweta, vijiji ambavyo pia vinakabiliana na mashamba makubwa ya miti yanayomilikiwa na kampuni ya Green Resources. Lengo la safari hii ilikuwa ni kujifunza juu ya athari zinazoletwa na uwepo wa mashamba makubwa ya miti katika maeneo hayo.

Kampuni ya Green Resources nchini Tanzania

Mashamba makubwa ya miti yaliaanza kupandwa katika maeneo hayo miongo kadhaa iliyopita, kwa mara ya kwanza mashamba hayo yalianzishwa na kampuni ya serikali iitwayo Sao Hill, na baadaye kuanzia miaka ya 1990, mashamba makubwa ya miti yalianza kuongezeka kupitia makampuni binafsi. Kampuni kubwa binafsi inayofanya kazi za upandaji wa mashamba makubwa ya miti ni kampuni ya Green Resources, ambayo ni kampuni ya Kinorway, inayomilikiwa kwa sehemu kubwa na taasisi ya serikali ya Norway inayoshughulikia masuala ya maendeleo inayoitwa Norfund. Pia kuna wawekezaji wakubwa wenye hisa zao katika kampuni hiyo. (1)

Kampuni ya Green Resources inajieleza kuwa ndio kampuni kubwa inayoendeleza ‘misitu’ na inayochakata mbao na bidhaa zake katika Afrika ya Mashariki, huku ikiwa na mashamba makubwa ya miti huko Msumbiji, Uganda, na Tanzania. Nchini Tanzania kampuni ya Green Resources inamiliki eneo lenye ukubwa wa hekta 74,850 ambapo kati ya hizo hekta 17,000 zikiwa zimeshapandwa tayari miti aina ya mikaratusi na paina. Kampuni hii inakiri katika tovuti yake kuwa “inaamini upandaji wa miti ni moja kati ya njia makini zaidi ya kuboresha hali za kijamii na kiuchumi kwa watu waishio vijijini na kwamba kampuni inalenga kuwa ndio mwajiri na mshirika anayependwa zaidi na wanajamii katika maeneo hayo.” Pia kampuni hii inaeleza kuwa kwa upande wa Tanzania “Eneo lililotumika kwa upandaji wa miti ni eneo lenye thamani ndogo na lenye nyasi tupu na ambalo limepatikana toka kwenye vijiji.”

Kinyume na ilivyo huko Msumbiji ambapo kwa sasa kampuni hii imepoteza hati yake (cheti), huko Tanzania, kampuni hii imepata hati toka FSC (Forest Stewardship Council), hati ambayo inairuhusu kampuni hii kudai kuwa mbao zake au mazao yake mengine ya miti yanatoka katika vyanzo ‘endelevu.’ Pia kampuni hii imeyasajili na kuyathibitisha mashamba yake ya miti kwa ajili ya utunzaji wa hewa ukaa (kupitia mfumo unaojulikana kwa kifupi kama VCS), na pia mashamba hayo pia yapo chini ya utaratibu ujulikanao kama CCBS, ambao pamoja na mambo mengine, kampuni inadai kuwa “utume wake” ni “ kuhamasisha na kukuza shughuli za usimamizi bora wa ardhi ambazo kwa hakika zinapunguza mabadiliko ya tabia-chini duniani, na kwamba zinaboresha maisha na kupunguza umaskini kwa jamii za vijijini huku zikihifadhi bayo-anuai.” (2)

Kampuni ya Green Resources iliwasili kwa wanajamii ya Idete mwaka 1996, Mapanda mwaka 1997 na Taweta mwaka 2007. Wanajamii walilaghaiwa kisha wakakubali kuingia mkataba wa makubaliano na kampuni ambayo ilifanikiwa hatimaye kuchukua eneo kubwa sana kiasi cha theluthi ya ardhi ya wananchi kwa kipindi cha miaka 99. Jambo hili lilitokea kutokana na sababu kuu mbili. Kwanza, wakati huo wananchi hawakufahamu umuhimu wa maeneo ya ardhi yaliyotolewa ama kukodishwa kuwa yana umuhimu sana kwao na wala walikuwa hawafahamu thamani halisi ya maeneo hayo. Lakini sababu nyingine kuu iliyowafanya kuikubali na kuipokea kampuni ya Green Resources ni orodha ya ahadi nyingi zilizotolewa na kampuni ya Green Resources. Kwa kuanzia, moja kati ya ahadi hizo ni ajira, pamoja na maboresho mengine ya miundo-mbinu ya vijiji; kama vile kujenga na kukarabati madarasa, kumbi na ofisi za serikali za vijiji, zahanati, vyanzo vya maji, pamoja na makazi ya wafanyakazi wa afya na walimu. Pamoja na ahadi hizo pia kampuni iliahidi kuwapatia asilimia 10 ya mapato yatokanayo na mauzo ya hewa-ukaa ambayo kimsingi yanatokana na kiasi cha hewa ukaa ‘kilichohifadhiwa’ katika misitu ya paina na mikaratusi iliyopandwa na kukua vizuri katika vijiji hivyo vitatu. Kampuni ya Green Resources iliweka ahadi hizi kwa maandishi na kisha ikasaini mikataba ya nyongeza na wanajamii kwa ajili ya malipo yatokanayo na mauzo ya hewa ukaa huku wananchi wakiwa hawafahamu sawasawa jinsi mfumo wa masoko ya hewa ukaa unavyofanya kazi.

Kwa sasa, baada ya kuwa kampuni hii imewasili miaka mingi iliyopita, wananchi wamekatishwa tamaa na wana hasira. Wananchi wanakiri kuwa ahadi nyingi za kampuni ya Green Resources hazijatekelezwa na badala yake ni ahadi chache tu zilizotekelezwa. Kwa sasa, hakuna ajira zozote zile za kudumu zilizotengenezwa. Katika vijiji vya Idete na Taweta, kampuni ya Green Resources imetengeneza ajira moja tu ya kudumu, na katika kijiji cha Mapanda ambacho kwa mujibu wa serikali ya kijiji kina idadi ya wakazi 5,503 – hakuna hata ajira moja ya kudumu. Pia wanavijiji wana malalamiko mengi sana kuhusiana na mazingira ya kufanyia kazi, ikiwemo mishahara midogo, ukosefu wa usafiri kwa wale walioajiriwa kwa ajira za muda mfupi; ikiwemo ukosefu wa vifaa maalumu vya kujikinga dhidi ya sumu zilizo katika pembejeo za kilimo. Pa wanavijiji wanailaumu kampuni ya Green Resources kwa kutowasilisha/kulipa michango yao ya mafao kwa mamlaka husika huku wao wakiwa wamekatwa hizo fedha toka katika mishahara yao kwa ajili ya kuchangia katika mifuko hiyo ya mafao ya kijamii.

Wanavijiji wanakiri kuwa baadhi ya miundo mbinu iliyo ahidiwa imetekelezwa. Lakini wakati huo huo katika kijiji cha Mapanda, bado wanakijiji wanangojea ukumbi wa mikutano na ofisi mpya kama ilivyoahidiwa na kampuni. Hatimaye kampuni ya Green Resources imeahidi kujenga ukumbi huo mpya mwaka huu baada ya kuwa imepata shinikizo la kutosha toka kwa wanajamii. Hata hivyo, hadi kufikia mwisho wa mwaka 2018 ukumbi huo ulikuwa bado haujajengwa wala kukamilika. Katika kijiji cha Taweta, jambo pekee ambalo wanakijiji wanalikumbuka ni ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa. Ofisi ambayo ilijengwa na kampuni ya Green Resources katika kijiji hiki kwa ajili ya kusimamia mashamba makubwa ya miti katika eneo hilo imefungwa na inaonekana kuwa imetelekezwa.

Mauzo ya hewa ukaa yalitolewa gawio kwa kijiji cha Mapanda peke yake, ambapo wananchi walipokea malipo ya hewa ukaa kwa kiasi cha fedha za Tanzania milioni 30 na millioni 33, malipo hayo yalifanyika mwaka 2011 na mwaka 2014. Malipo hayo yaliyofanyika kwa ujumla wake yanafikia kiasi cha dola za kimarekani elfu 40, kiasi ambacho ni kidogo sana kwa kijiji chenye watu zaidi ya elfu 5 huku kikiwa na changamoto kubwa ya miundo mbinu kama vile uhitaji wa kuboresha mfumo wake wa maji safi. Pamoja na hayo, hakukuwa na uwazi kuhusiana na namna kiwango hicho cha fedha kilicholipwa kwa wanajamii kilivyopatikana. Wananchi walikuwa hawafahamu thamani halisi ya mauzo ambayo kampuni imepata kutokana mauzo ya hewa ukaa iliyohifadhiwa katika eneo lao, pia walikuwa hawafahamu ikiwa fedha walizolipwa ni asilimia 10 au la ya mauzo ya hewa ukaa ambayo kampuni ilikuwa imepata. Vijiji vya Idete na Taweta havijapokea malipo yoyote yale kutokana na mauzo ya hewa ukaa hadi sasa. Katika mada iliyowasilishwa na kampuni ya Green Resources kwa ajili ya watu wote inayopatikana katika mtandao wa intaneti (3), kampuni inalalamika kuwa “malipo ya hewa ukaa yanakatisha tamaa”, lakini kampuni inaeleza kuwa hata hivyo kampuni ya “Green Resources imezalisha au kupata dola za kimarekani millioni 2 (…)”. Ikiwa mtu atapiga hesabu ya asilimia 10 ya kiasi hicho cha fedha, basi ni dhahiri kuwa wanakijiji walipaswa kupokea walau dola za kimarekani laki 200 – kiasi ambacho ni kikubwa zaidi kuliko kiasi ambacho wanakijiji wa Mapanda walilipwa.

Wanajamii katika vijiji vitatu tulivyovitembelea wanajuta kutoa ardhi yao kubwa kwa kampuni hii na kwamba kwa sasa wanazuiwa kuingia katika ardhi hiyo hata kwa shughuli ya kukusanya au kukata nyasi au kuchimba udongo wa mfinyanzi katika maeneo ambayo bado hata hayajapandwa miti. Walipoulizwa ikiwa wanakubaliana na madai ya kampuni kuwa ardhi waliyotoa ina ‘thamani ndogo’ na kwamba ilikuwa ‘imeharibiwa’ (kama ambavyo kampuni ya Green Resources na makampuni mengine ya upandaji miti wanavyodai), wananchi walijibu kwa pamoja kuwa madai hayo ni uongo mkubwa. Wananchi wanafahamu kuwa ardhi hiyo ni ya thamani sana, yenye rutuba, na ambayo ni muhimu kwao na hatma yao ya baadaye. Kwa sasa ikiwa wanataka kuingia katika ardhi hiyo ni lazima waombe kibali cha kufanya hivyo. Katika kijiji cha Idete, wananchi wanahofia kuwa wanashindwa kukusanya au kuvuna aina fulani ya magugu yanayojulikana kwa lugha ya kienyeji kama (Milulu) yanayotumika kutengenezea vikapu vya asili ambavyo hutengenezwa zaidi na wanawake. Pia mwanakijiji mmoja mwanamke anahofia juu ya ongezeko la maambukizi ya VVU/UKIMWI kutokana na ongezeko la wafanyakazi toka nje ya maeneo ya kijiji cha Idete.

Mwanakijiji mwingine anadai kuwa hakuna namna ya kuweza kulinganisha manufaa waliyoyapata hadi sasa dhidi ya hasara na taabu ambazo wananchi wanazipata baada ya kuitoa na kuikodisha ardhi yao kwa miaka 99. Kwa hakika wanakijiji walio wengi wanahofia sana maisha yao ya baadaye. Mwanamke mmoja wa kijiji cha Idete alitafakari kwa kina na kwa huzuni juu ya hatma ya watoto wake ikiwa watapata ardhi ya kulima hapo baadaye, na alisema kwa hali ilivyo ana hakika kuwa wajukuu zake watakosa eneo la kuzalisha mazao ya chakula na kufugia mifugo na kwamba kwa sababu hiyo umaskini utaongezeka sana.

Sio jambo la kushangaza, kwa sasa wananchi katika vijiji vitatu wanataka ardhi yao inayomilikiwa na kampuni ya Green Resources irudishwe kwao au angalau sehemu ya ardhi irudi mikononi mwao. Huku wakitafakari juu ya hatma yao ya baadaye, wananchi wengi katika vijiji hivyo wanataka kuwa na uhakika kuwa watakuwa na ardhi ya kutosha kwa idadi kubwa ya wanavijiji katika jamii zao, yaani miaka michache ijayo. Hivyo hivyo wanavijiji hao wanakabiliana na changamoto kubwa kwa kuwa wamesaini mikataba ya kisheria ambapo wamekubali kukodisha ardhi zao za vijiji kwa kampuni hiyo ya Green Resources. Lakini, mikataba hiyo ina uhalali gani ilhali ilikubaliwa kwa msingi wa orodha ya ahadi nyingi ambazo hazijatekelezwa huku shughuli za kampuni hiyo zikiendelea kuweka hatma ya baadaye ya wananchi hao mashakani?

Mambo yaliyogunduliwa katika safari ya kutembelea vijiji hivyo yanatoa msingi wa kutoa hoja ili kuhoji ukweli wa maelezo ya kampuni pale inaposema kuwa nchini Tanzania kampuni inafanya kazi vizuri na kwamba ni mshirika anayependwa zaidi na wanajamii wa maeneo ya vijijini.

Taarifa ni Nguvu

Habari hizi kuhusu kampuni ya Green Resources nchini Tanzania inaonyesha kuwa makampuni ya upandaji miti wanachohitaji wakati wote ni kupata ardhi kubwa ili waweze kufanya shughuli zao. Pia inaonyesha jinsi ambavyo makampuni haya yanafanya hivyo kwa msingi wa kutoa ahadi za uongo au ahadi zinazotekelezwa vibaya kwa nia tu ya kuwashawishi wananchi ambao hatimaye huathirika kwa kuikodisha ardhi yao. Maelezo na uzoefu toka kwa jamii zinazokabiliana na kampuni ya Green Resources na makampuni mengine ya mashamba ya miti ni muhimu sana kwa vijiji vingine ili viweze kujifunza na kutafakari vizuri.

Wanakijiji wa Nzivi waliweza kuyafahamu haya kwa wakati na walipata uzoefu toka katika vijiji vingine hasa walipokuwa wakiongea na vijiji jirani, na wakawa na mashaka kuwa na wao wasije wakakutana na hali kama hiyo ya kusikitisha, na kwa msingi huo waliamua kutoziamini ahadi za makampuni na wakaamua kusema hapana kwa kampuni yoyote ile inayotaka kupata kiwango kikubwa cha ardhi yao kama vile Green Resources. Waliamua kubakia na usimamizi na uthibiti wa ardhi yao kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Hii haimaanishi kuwa wanakijiji wa Nzivi hawawezi kupokea uwekezaji wowote ule. Viongozi wa kijiji walitueleza kuwa wametenga eneo dogo la ardhi ya kijiji kwa ajili ya wawekezaji, na kwamba eneo hilo ni maalum kwa wawekezaji wasiohitaji eneo kubwa la ardhi yao na walio tayari kusaidia na kuunga mkono huduma za kijamii ambazo ni muhimu na hazipo kama vile elimu na afya. Wananchi wanaamini kuwa aina hiyo ya uwekezaji usiohitaji ardhi kubwa na unaounga mkono huduma za kijamii ni wa muhimu sana maana utaendelea kulinda haki ya kumiliki ardhi yao, misitu, na mbuga zenye nyasi vitu ambavyo wanavitegemea katika maisha yao ya kila siku.

Jambo la ajabu, hakuna mwekezaji aliyeonekana kutoa ombi kwa wananchi wa kijiji hicho. Hii inaonyesha jinsi wawekezaji waliogubikwa na nia ya kupata faida kama vile kampuni ya Green Resources na wadau wake wasivyokuwa na nia ya kusaidia mahitaji ya watu wa vijijini nchini Tanzania kama ilivyo kwa kijiji cha Nzivi.

Justiça Ambiental! - Mozambique, SUHODE Foundation - Tanzania na WRM

http://www.suaire.suanet.ac.tz:8080/xmlui/bitstream/handle/123456789/1659/SAID%20ASIAD.pdf?sequence=1&isAllowed=y
http://www.greenresources.no and http://www.climate-standards.org/about-ccba/
http://www.greenresources.no/Portals/0/pdf/GR_NewForest_for_Africa_170316_(new).compressed.pdf