(Swahili) Kuuhuisha Ustawi: Vijiji vya Kochi taluka, nchini India, wanapinga uchimbaji wa madini na wanafungua nafasi kwa ajili ya uongozi binafsi (1)

Mikutano ya vijiji (Kwa Kihindi: Gram Sabhas) huko Korchi taluka, wilaya ya Gadchiroli, jimbo la Maharashtra, India, pamoja na upinzani wa wanajamii dhidi ya uchimbaji madini unaofadhiliwa na serikali ya jimbo, wanafanya kazi ya kuzihuisha na kuzijenga upya taasisi za kiuongozi za serikali za mitaa. Mikutano ya vijiji (Gram Sabhas) 90 kati ya 133 katika eneo la Korchi taluka (Taluka: ni aina fulani ya ngazi ya usimamizi wa serikali) zimeungana na kuunda shirikisho la mikutano ya vijiji wanaloliita kwa lugha ya kihindi Maha Gramsabha (Maana yake Gram Sabha kubwa).

Wakati huo huo, muungano wa vikundi vya wanawake pia vimeanza kuzipasa sauti zao ili ziweze kusikika sio tu kwa lengo la kupinga uchimbaji madini bali pia kupinga aina mpya za ufanyaji maamuzi katika taasisi za ngazi za vijiji na taluka, ikiwemo Maha Gramsabha. Vikundi hivi vinajitokeza kama majukwaa ya kupinga uchimbaji madini, kupanga mikakati, kupanga masharti na kanuni za usimamizi wa misitu na uhifadhi, kumiliki njia mbalimbali zinazowawezesha kuishi pamoja na vyanzo vingine vya kiuchumi, kufufua utambuzi wao wa kiutamaduni, kukuza usawa wa kijamii, kupaza sauti moja kwa moja na kukuza demokrasia ya kijinsia, na kuhoji mifumo iliyopo ya maendeleo. Makala hii inajaribu kuonyesha jinsi mchakato huu unavyozidi kujifunua.

Upinzani na Kujipanga toka ngazi za chini

Pamoja na kuwa watu wanasimamiwa na utawala wa Wilaya ya Gadchiroli ikisaidiana na Panchayats waliochaguliwa (Panchayats maana yake ni kamati tendaji inayohusisha kijiji kimoja au zaidi ambayo ndiyo kitengo cha kwanza cha utawala katika mfumo wa kiutawala wa India uojulikana kama Panchayati Raj, yaani serikali za mitaa zinazojitegemea), watu wa Korchi taluka wameendelea kuwa na aina zao nyingine za kiusimamizi ambazo si rasmi na ambazo ni za kimila zinazoitwa Gram Sabhas na Ilakas (zinazohusisha maeneo yanayohusisha vijiji vingi), mifumo hii isiyo rasmi ya watu wa Korchi inasimama kama miundo ya kiuongozi katika ngazi ya kijiji na ngazi ya juu ya kijiji. Hali zikiwa na mamlaka kidogo ya kisiasa na kiuchumi, taasisi hizi ambazo si rasmi hadi hivi karibuni zilikuwa zimejikita katika masuala ya kijamii na kiutamaduni na katika kusuluhisha migogoro. Eneo la Korchi taluka lina taasisi hizo zisizo rasmi yaani Ilakas tatu ambazo ni Kumkot, Padyaljob, na Kodgul; zikiwa na jumla ya Gram Sabhas 133 zenye wakazi wapatao 43,000 (kati ya hao asilimia 73 ni kutoka jamii za makabila ya kiasili ya Gond na Kanwar).

Karibia asimilia 85 ya wilaya ya Gadchiroli imegubikwa na misitu. Na takribani watu wote wanaoishi katika eneo hilo wanategemea sana misitu kwa maisha yao kwa maana ya kupata fedha na pia kupata chakula cha kujikimu. Pamoja na kuwa misitu ni ya maana sana kwa ajili ya uchumi wa watu wa chini na kwa maisha yao, bado misitu hiyo hiyo ni sehemu muhimu sana ya maisha ya kijamii na kidesturi kwa watu wa kabila la kiasili la adivasi, pia ni sehemu ya utambulisho wao wa kisiasa. Pamoja na ukweli huo hadi hivi sasa watu wengi katika eneo hilo wamewekewa vikwazo na wanaruhusiwa kutumia hiyo misitu kwa mbinyo kwa sababu ya utaratibu wa kikoloni unaotokana na sera na sheria zake za usimamizi wa misitu, kumekuwepo na ukiritimba ambao umesababisha desturi ya rushwa na maovu kwa mtu anayetaka kuutumia msitu. Misitu hii pia ni muhimu sana kwa serikali ya jimbo. Uziduaji wa kukata mbao kibiashara na mazao mengine ya msituni vimekuwa vikifanyika na idara ya misitu kupitia ukodishaji kwa wakandarasi na kwa makampuni ya karatasi na rojorojo za miti za kutengenezea vifaa vya ujenzi, na hivi karibuni ukodishaji umekuwa ukifanyika kwa makampuni ya uchimbaji madini.

Kwa miongo mingi, watu wa Gadchiroli wamekuwa wakizipinga sera kandamizi na zenye ubaguzi, pamoja na rushwa na maovu yanayofanywa kwa makabila ya wenyeji. Na pia wanapinga uchimbaji wa sasa wa madini unaofadhiliwa na serikali ya jimbo. Kati ya mwaka 1990 na 2017, leseni 24 za ukodishaji kwa ajili uchimbaji wa madini zimetolewa au kupendekezwa na Wilaya, kwa pamoja leseni hizo zimeleta athari katika eneo la takribani hekta 15,000 za misitu mizito na zaidi ya hekta 16,000 zilizoathirika kidogo. Katika eneo la Korchi taluka pekee, takribani leseni 12 za uchimbaji wa madini zilipendekezwa pamoja na kuwepo upinzani mkubwa na imara toka kwa wananchi, matokeo yake ni kuwa leseni hizo ziliathiri zaidi ya hekta 1032.66.

Baada ya mapambano ya wananchi kwa muda mrefu katika sehemu mbalimbali za India dhidi ya sera za kibaguzi, kandamizi, na sera za upande mmoja toka juu hadi chini ikiwemo sera mbaya za uhifadhi; basi kufuatia mapambano hayo mwaka 2006 serikali ilisalimu amri na kulilazimu Bunge la India kupitisha sheria ya kihistoria inayojulikana kama: Sheria ya Makabila Yaliyopangwa na Wakazi Wengine wa Kiasili wa Misituni, 2006 (Kwa Kiingereza: The Scheduled Tribes and Other Traditional Forest Dwellers (Recognition of Rights) Act 2006, pia sheria hii inajulikana kama Sheria ya Haki za Msitu ya India (Kwa Kiingereza: Forest Rights Act of India (katika makala hii sheria hii itaandikwa kwa kifupisho hiki FRA). Sheria ya FRA imetoa mwanya wa kuzitambua aina 14 za haki mbalimbali za misitu za kiasili kwa makabila yaliyopangwa na kwa wakazi wengine wa kiasili wa misituni. Moja kati ya mambo muhimu yaliyotambuliwa na sheria hii ni pamoja na Gram Sabhas kuwa na haki ya kutumia, kusimamia, na kuhifadhi misitu yao ya kiasili na kuilinda misitu hiyo dhidi ya vitisho vya ndani na vya kutoka nje. Sheria hii pia inalazimisha uwepo wa mashauriano huru, ya mapema kabla, na ridhaa yenye taarifa sahihi toka kwa Gram Sabhas kabla ya misitu yao ya kiasili haijabadilishwa matumizi kwa madhumuni ambayo si ya misitu. Kati ya vifungu muhimu kabisa katika sheria hii na ambacho ni muhimu sana ni ufahamu mkubwa wa kutumia kitengo cha uongozi cha Gram Sabha – ambacho kinaweza kutambuliwa na kikundi cha watu wanaoishi katika eneo ambalo linaweza lisiwe na sifa ya kuitwa kijiji katika rekodi za serikali.

Kuziwezesha Gram Sabhas

Baada ya kampeni endelevu inayohusu haki ya kutumia, kusimamia, na kuhifadhi misitu yao ya kiasili, kuanzia mwaka 2009 hadi 2011 Gram Sabhas 85 za Korchi taluka zilitambuliwa. Utambuzi huu ulisaidia kuziwezesha Gram Sabhas kusimamia misitu yao na kuitumia kwa namna ya uendelevu, kwa kuwa katika mazingira hayo ni dhahiri kuwa wananchi wanao umiliki wa misitu.

Baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa, hasa kutoka vijijini ambao wamepokea haki hizi maalum lakini ambao pia walikuwa wakikabiliana na vitisho toka kwenye miradi ya uchimbaji wa madini, walitumia fursa hii kufahamu jinsi sheria hii ya FRA inavyoweza kuziwezesha Gram Sabhas. Na pia kuwahamasisha wananchi ili wafahamu jinsi Gram Sabhas iliyowezeshwa kisheria inavyoweza kufanya kazi kuelekea utambuzi binafsi na usimamizi binafsi, ikiwemo kudai mamlaka kubwa inayojali usawa katika kusimamia misitu na uchumi wa watu wa ngazi ya chini. Mikutano ya kwenye ngazi ya Taluka inasaidia uwepo wa majadiliano ya kina kuhusu utendaji, haki, mamlaka, na majukumu ya Gram Sabha. Hadi kufikia mwaka 2017, vijiji 90 huko Korchi taluka walikuwa wamejipanga upya na kuziimarisha Gram Sabhas za vijiji vyao ili ziweze kuwa ni vyombo vyenye kufanya maamuzi shirikishi, na vyenye kuzingatia uwazi na uwajibikaji katika ngazi ya vijiji. Kila Gram Sabha ilifungua akaunti ya benki, walichagua katibu na mwenyekiti. Hawa wasimamizi wa ofisi wana majukumu ya kuwasiliana na maofisa wa serikali na wadau wengine wa nje. Gram Sabhas zilianza kujadiliana na kutangaza bidhaa zao za mazao ya msituni ambazo si mbao. Faida inayopatikana ilianza kwenda moja kwa moja kwa Gram Sabhas, ambayo iliwajibika kuwalipa wafanyakazi (familia zote katika kijiji), na walikuwa wanabakiza kiasi fulani cha asilimia kwa ajili ya akaunti ya kijiji na fedha iliyobakia iligawanywa kama faida kwa wakusanyaji wa fedha. Hadi wakati huo, Gram Sabhas, ambazo kimsingi zilikuwa zimedhoofika kiuchumi na kiuwezo zilianza kuyapata mambo hayo mawili, yaani uwezo na uchumi. Kwa mfano, mwaka 2014 Gram Sabhas zilikuwa na mapato sifuri, lakini ilipofika mwaka 2017, Gram Sabhas 87 zilikuwa na jumla ya mapato yaliyofikia zaidi ya Rupia milioni 120 (sawa na Dola za Kimarekani - US$ 1,700,000).

Hadi kufikia mwaka 2016, Ilakas za kimila zilianza kujiona kuwa zenyewe ni kama ngazi ya juu kuliko Gram Sabhas. Hivyo, hizi Ilaka za kimila (Mikutano) zilianza kujumuisha majadiliano ya kuziwezesha Gram Sabhas, demokrasia ya moja kwa moja, kujitambua, sheria ya FRA, uchimbaji wa madini na athari zake, ukuaji na maendeleo, ukoloni na ubeberu, na mambo mengine. Pia kulifanyika juhudi za kurejelea maana ya neno ‘adivasi’ (kabila la kiasili), utamaduni wa adivasi na historia yake, na kuelezea kwa upya mapinduzi na mabadiliko ya mashujaa wa kikabila (historia ambayo haionekani katika historia za kawaida) na kufahamu ombwe la ufahamu kuhusiana na utamaduni na imani ya kabila la adivasi katika dini nyingine kuu.

Maha Gramsabha – Shirikikisho la Gram Sabhas

Kadri Gram Sabhas zilipoanza kupata nguvu kutokana na uwezeshaji na utambuzi, basi ilikuwa ni muhimu sana kwao kujiunga na kuwa na nguvu zaidi ili kuwasaidia wale ambao walikuwa bado wanaanza ili wajipange na ili wawe na ufahamu wa pamoja na usaidizi. Ili kuvuna mazao ya misitu ambayo si ya mbao na kuweza kuyauza kunahitaji stadi na uelewa, ufahamu, na nguvu ili kuweza kukabiliana na nguvu ya soko. Lakini pia ili kuweza kushughulikia mikakati inayoleta utengano ya makampuni ya uchimbaji wa madini kunahitaji kuwa na matendo ya nguvu ya pamoja.

Ilaka sabhas za kimila zilikuwa na ukomo wake hasa katika kuyashughulikia mambo haya. Hivyo mwaka 2017, shirikisho la Gram Sabhas 90 liliundwa ili kuhakikisha kuwa masoko hayawanyonyi wadhaifu, na ili kuwepo na usawa katika kugawana faida na kugawana maarifa, na ili kushikana mikono pamoja. Kwa sasa Maha Gramsabha (MGS) ni mahali pa kisiasa, kiuchumi, kijamii, na kiutamaduni ambapo panalenga kutambuliwa na wananchi katika suala zima la utawala. Kila Gram Sabha inachagua wanawake 2 na wanaume 2 ili kuwa wakilisha katika MGS, pia kila Gram Sabha inapitisha azimio la kujiunga na MGS na kutii miongozo na kanuni zake. Wawakilishi wote waliochaguliwa wanatakiwa kutoa mrejesho kwenye Gram Sabhas wanazotoka. Na ikiwa kuna sera mpya imetolewa na MGS basi huwa inajadiliwa kisha hufanyiwa maamuzi kulingana na uelewa na taarifa walizonazo, lakini mambo hayo yote ni lazima yafikishwe kwenye Gram Sabhas kwa uthibitisho. Kabla ya kuikubali sera yoyote ile, wawakilishi hujadiliana juu ya mambo yanayohitaji utekelezaji na pia huwa kunakuwa na mjadala kuhusiana na gharama zilizotumika.

Wanawake, uchimbaji wa madini, na majukumu ya muungano wa vikundi vya wanawake

Katika jamii ya leo ambayo imeelemewa na mfumo dume, ni dhahiri kuwa wanawake hawana sauti kubwa katika vijiji vya kimila na katika usimamizi wa misitu. Pia wanawake walikabiliana na changamoto nyingi za kijamii, ikiwemo unyanyasaji na vurugu katika ngazi ya kaya ikichangiwa na ulevi, ukosefu wa rasilimali, na ukosefu wa haki katika kufanya maamuzi.

Hali wakiungwa mkono na AZAKI inayoitwa Amhi Amchi Arogyasaathi, taratibu kabisa vikundi vya wanawake (parishads) vilianza kufuatilia utekelezaji wa sheria na mipango ambayo itasaidia kuwwezesha wanawake. Vikundi hivi vya wanawake - parishads vilijikuta vinakuwa ni kundi kubwa la kuwasaidia wanawake wanaokabiliana na ukiukwaji wa haki, unyanyasaji, vurugu na mambo mengine yoyote yale katika ngazi ya familia au jamii kwa ujumla. Kadri uelewa ulivyozidi kuongezeka miongoni mwa wanawake, na kadri walivyozidi kupata ujasiri wa kupaza sauti na kutoa maoni yao, hapo ndipo wanawake wengi sana walipoweza kusema hadharani kuwa ustawi wao na wa familia zao unahusishwa sana kwa karibu na ustawi wa misitu. Hivyo, ilikuwa ni lazima kwa wanawake kujadili suala la uharibifu wa misitu na haki ya kuweza kuitumia misitu na kuilinda.

Jambo hili lilionekana kuwa ni muhimu sana kwa wanawake mwaka 2009, hasa katika vijiji ambavyo viligundua kuwa misitu yao ya kiasili imetolewa na kukodishwa kwa ajili ya uchimbaji wa madini. Kupitia vikundi hivyo - parishads, wanawake walikuwa ni sehemu ya nguvu kubwa ya upinzani dhidi ya uchimbaji wa madini. Upinzani wao wa kimwili na uwezo wa kujieleza katika mikutano mbalimbali dhidi ya uchimbaji wa madini, ikiwemo mashauri yaliyokuwa yamefadhiliwa na serikali, basi jitihada hizo zote zilisababisha vibali vya ukodishaji kwa kazi ya uchimbaji wa madini kusimamishwa hadi leo hii huko Korchi taluka. Hatimaye, kupitia vikundi vyao parishad, wanawake waliweza kuwa na majadiliano kadhaa kuhusiana na athari za uchimbaji wa madini katika maisha yao, familia zao na misitu yao, ikiwemo haja ya kuilinda misitu. Pia vikundi hivyo vya parishads vimekuwa ni muhimu sana katika kuwakuza na kuwainua wanawake viongozi katika majukwaa mbalimbali ili kuelezea mapambano yao na maoni yao, ikiwemo fikra yao kuhusu ustawi, ambayo inahusishwa kwa ukaribu kabisa na misitu yenye afya.

Wakati wa kipindi cha upinzani dhidi ya uchimbaji madini katika eneo la Korchi taluka, wanawake viongozi katika vikundi vya parishads walianza kutambua na kujadili kuhusu uhalisia uliokuwepo ambapo wanawake wanakuwa mstari wa mbele katika upinzani ilhali hawana nafasi katika utaratibu wa kimila unaohusisha mchakato wa maamuzi kuhusu misitu. Hadi kufikia mwaka 2015, majadiliano kwenye ngazi ya Gram Sabhas kama vitengo vya uongozi vilikuwa vinaanza kupata nguvu, katika kipindi hicho mikutano ya ngazi ya taluka ilikuwa inaandaliwa, utekelezaji wa sheria ya FRA ulikuwa unazungumziwa katika ngazi mbalimbali za mikutano ya taluka na Ilaka. Hata hivyo, hakuna aliyekuwa anaangalia masuala ya ushiriki wa wanawake, haki za wanawake chini ya sheria hiyo na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kutokana na mazao ya misitu. Baadhi ya wanawake viongozi walianza kushiriki katika mikutano ya ngazi ya taluka.

Katika moja ya mikutano ya kwanza ya Maha Gramsabha, wanachama wa parishad walisisitiza kuwa pamoja na kupinga ukiritimba unaoletwa na matabaka kandamizi, ilikuwa ni muhimu pia kupinga mifumo ya mila na desturi iliyokuwa ina halalisha maonezi kwa wanawake ikiwemo kuwazuia wanawake katika ufanyaji wa maamuzi, ikiwemo maamuzi kuhusiana na misitu. Walihakikisha kuwa MSG inajumuisha wawakilishi 2 wanawake na wanaume 2 toka katika kila Gram Sabha. Kitendo cha kuwa na kitengo cha kwanza cha maamuzi cha Gram Sabhas katika vijiji vyao kulitoa fursa zaidi ya ushiriki wa wanawake kuliko muungano wa vikundi vya wanawake pekee yaani parishads, ambao uko mbali na kijiji. Kupitia juhudi zilizofanywa na parishads, baadhi ya Gram Sabhas zimefanya juhudi ya kipekee kuhakikisha mikutano inafanyika wakati ambapo wanawake wanaweza kushiriki. Vikundi vya wanawake vya parishads pia vilihakikisha kuwa Korchi taluka ni moja kati ya ngazi chache za kiutawala nchini ambapo haki za wanawake kwa mujibu wa sheria ya FRA zinazingatiwa. Sheria ya FRA inatoa mwanya na uwezekano wa kumiliki ardhi kwa pamoja kati ya mke na mume. Katika vijiji vingi vya Korchi, hati nyingi za umiliki wa ardhi zimetolewa kwa pamoja ikiwemo baadhi ambazo zipo kwa majina ya wanawake kama wamiliki wa kwanza na mahali pengine wanawake kama wamiliki pekee wa ardhi.

Hali wakipiga hatua mbele, Gram Sabhas nyingi zimefanya maamuzi kuwa wanawake watapata mshahara wa kila siku kwa kazi wanazofanya pamoja na faida toka kwenye mauzo ya mazao ya msituni ambayo si ya mbao moja kwa moja katika akaunti zao badala ya fedha hizo kulipwa katika akaunti za waume zao. Kusema kweli, kijiji kimoja kinachoitwa Sahle kimeamua kuwa faida yote inayopatikana katika familia toka katika mazao ya misitu itaenda katika akaunti ya wanawake wa familia hiyo – maamuzi ambayo ni makubwa na ya kipekee.

Hitimisho

Mchakato wa kudai haki, utawala na uongozi binafsi na usimamizi wa misitu katika eneo la Korchi bado upo katika hatua zake za awali na unazidi kujifunua vizuri na kwa usawa. Mambo kadhaa ambayo yamekuwa ni chachu ya kusaidia mchakato huo yamesaidia sana katika kuimarisha upinzani, utawala binafsi, ikiwemo madai ya dhana ya ustawi wa jamii katika eneo la Korchi. Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na historia ndefu ya kujipanga kisiasa na mijadala kuhusu ‘maendeleo’, jambo ambalo limetoa nafasi kwa uongozi imara wa ngazi ya chini wa wanaume na wanawake; uwepo wa viongozi wa kipekee ambao wamesababisha uwepo wa mijadala ya kiitikadi na hotuba mbalimbali; uwepo wa nafasi za kisheria zilizotolewa na sheria wezeshi kama ile ya FRA; kubadilishana uzoefu kati ya watu na watu; faida kubwa za kiuchumi baada ya kuugatua uchumi wa mazao ya misitu ambayo si mbao kwenye ngazi za chini; usaidizi wezeshi na usio ingilia toka mashirika mbalimbali na wanaharakati binafsi.

Mambo hayo yamesababisha uwepo wa umakini wakati wote, wepesi, na mchakato unaohusisha vitu mbalimbali katika kushughulikia changamoto za ndani na za nje. Hii inajumuisha kushughulikia sera kandamizi na za kitabaka, ikiwemo matumizi ya nguvu nzito za kijeshi na sera za uchumi mpana ambazo zinaegemea na kuyapendelea makampuni na kupendelea ubinafsishaji; ikiwemo kushughulikia matabaka na mfumo dume katika ngazi za chini. Kujumuisha sauti za wanawake katika ufanyaji maamuzi na katika mgawanyo wa faida kumesaidia kuwepo kwa uongozi wa kijamii wenye usawa, na hivyo kumefanya kuwepo na upinzani imara dhidi ya uchimbaji wa madini, na usimamizi imara wa misitu na uhifadhi wake, na pia kumejitokeza dhana iliyo nzuri kuhusu ustawi wa wanajamii kama mbadala wa mfumo wa maendeleo unaojikita katika tasnia ya uziduaji.

Neema Pathak Broome, Shrishtee Bajpai na Mukesh Shende

Neema na Shrishtee ni wanachama wa Kalpavriksh, wanaishi Pune na Mukesh na wanafanya kazi na asasi ya Amhi Amchi Arogyasaathi, asasi iliyopo Gadchiroli

(1) Makala hii imejikita katika uchunguzi wa muda mrefu uliofanywa na Kalpavriksh, kwa ushirikiano na asasi ya Amhi Amchi Arogyasaathi (AAA) na Korchi Maha Gramsabha kama sehemu ya mradi wa Maarifa Yaliyotolewa na Wanaharakati-Wanazuoni kwa Ajili ya Haki ya Mazingira (Kwa Kiingereza: ACKnowl-EJ (Academic-Activist Co-Produced Knowledge for Environmental Justice). ACKnowl-EJ ni mtandao wa wanazuoni na wanaharakati ambao wanashughulika katika kuchukua hatua za utafiti shirikishi unaolenga kuibua mbinu nzuri za kuibadilisha jamii kama mbadala wa tasnia ya uziduaji (http://acknowlej.org/)