(Swahili) Jinsi ya Kuimarisha Mavuguvugu ya Upinzani?

Ni ukweli usiopingika kuwa misitu ya asili inaharibiwa sana kwa kiwango cha kasi sana. Ekari nyingi sana maelfu kwa maelfu zinaharibiwa ili kupisha miradi ya uchimbaji wa madini, uziduaji wa mafuta na gesi asilia, upandaji wa miti kama vile Mikaratusi au michikichi ya mafuta ya mawese, mabwawa ya kuzalishia umeme, utoaji wa vibali vya kukata magogo, na miradi mikubwa ya ujenzi wa miundo mbinu, na mambo mengine mengi.

Lakini pamoja na madhara mengi ambayo hakuna anayeweza kukana yanayotokana na shughuli hizi ulimwenguni kote, shughuli hizi pia zinasababisha ujio wa mambo mengine kujitokeza: na baadhi ya mambo yanayojitokeza ni pamoja na mavuguvugu mbalimbali yaliyo imara kutoka kwa wanajamii walioathiriwa wanaoyalinda maeneo yao, njia zao za kimaisha, tamaduni na imani zao, na hata uwepo wao.

Pamoja na ukandamizaji mkubwa wa kuwabambikizia watu kesi za jinai na vurugu mbalimbali toka kwa baadhi ya makampuni, pamoja na serikali za sasa kuruhusu vitendo hivi viovu kuendelea, pamoja na mawakala wa “maendeleo” na taasisi za fedha kuendelea kutoa fedha na kuunga mkono biashara hizo ili ziweze kuendelea; ukweli ni kuwa wanajamii na watu wengi hawajaacha kujikusanya, kujipanga, kuratibu na kupinga mauaji kwa jina la mfumo wa “maendeleo.” Pasipo mapambano haya, ni hakika kuwa misitu, vyanzo vya maji na maeneo mengine yataharibiwa kwa ukubwa zaidi.

Taarifa hii rasmi ya habari ni tafakari kuhusu mavuguvugu mbalimbali ya upinzani na changamoto kubwa sana zilizopo leo hii, na kuhusu changamoto zile zitakazokuja baadaye. Tunajiuliza: ni jinsi gani mavuguvugu haya ya upinzani na mashirika mengine katika ngazi ya jamii yanavyoweza kuimarishwa kwa lengo la kuzuia uharibifu wa misitu na watu katika muktadha wa sasa duniani?

Mahojiano na Kum’Tum wa jamii ya watu wa Akroá-Gamela, katika lango kuingilia kwenda misitu ya Amazon ya Brazili, yalitufikisha katika mchakato binafsi na wa pamoja ambapo suala la kuzirejelea kumbukumbu na kupaza sauti kama watu yalikuwa ni mambo makuu katika kujiunganisha na kudai ardhi na uhai. Kum’Tum anatukumbusha kuwa, "Hatudai ardhi kwa ajili ya uzalishaji tu. Tunaidai ardhi kwa kuwa ni mahali patakatifu; ni mahali panapotoa maana ya uwepo wetu.”

Kutoka Sierra Leone tunapata hadithi ya wanajamii wa Port Loko, ambao—baada ya takribani miaka kumi ya mapambano dhidi ya kampuni iliyokuwa imenyakua ardhi yao kwa njia za ulaghai na kisha ikaijaza ardhi hiyo kwa michikichi ya mafuta ya mawese—hatimaye mahakama imeamua ardhi hiyo irudishwe kwa wanajamii. Ni dhahiri kuwa mchakato wa uratibu kati ya mashirika ya wanajamii katika ngazi ya chini, katika kanda, na katika ngazi ya kimataifa unaonekana kuwa ni wa muhimu sana katika mapambano hayo. Kwa sasa wanajaribu kufikiria jinsi watakavyoitumia ardhi yao kubwa ambayo imegubikwa na mistari mingi ya michikichi ya mafuta ya mawese.

Kutoka India, kuna makala inayoangazia aina mbalimbali za kuyahuisha na kuyajenga upya mashirika ya kwenye ngazi za jamii katika mji wa Korchi, Mahrashtra. Kwa kutoa mkazo maalum juu ya wanawake kuungana, makala hii inaeleza jinsi walivyofanya sauti zao zikasikika—sio tu kwa lengo la kupinga uchimbaji madini bali pia kupinga aina mpya za ufanyaji maamuzi katika ngazi ya kijiji na ngazi za juu za kijiji. Baadhi ya vitendo wanavyovifanya ni kuwa vikundi hivi vingi vinatengeneza mikakati ya kuhifadhi misitu kwa usimamizi wao katika ngazi ya chini, wanaufufua utambulisho wao wa kiutamaduni, wanaikiri na kuithibitisha demokrasia ya moja kwa moja na demokrasia ya kijinsia na wanahoji juu ya mifumo ya sasa ya maendeleo.

Kutoka Amerika ya Kusini, kuna makala nyingine inayoangazia juu ya mashambulizi mengi kwa wanawake wanaolinda na kutetea maeneo. Makala hii inaelezea jinsi wanawake wanavyoweza kufanya matendo mbalimbali ambayo yamewawezesha kuisimamia na kuiweka hadharani mitazamo yao mbalimbali tena ya kipekee, na jinsi ambavyo kwa nyakati nyingi wameweza kuzuia au kusimamisha kwa muda shughuli za uziduaji. Wao wanakazia juu ya mchakato wa uponyaji kuwa ni jambo la msingi katika mjadala wa ufahamu kati ya watu, muktadha, na vizazi —na kutokea mahala pa uthibitisho wa kumbukumbu za wanawake wahenga.

Taarifa hii rasmi ya habari pia imejumuisha mahojiano na mwanaharakati wa Kikameruni na mtetezi wa haki za binadamu, Nasako Besingi. Besingi anatukaribisha kutafakari juu ya ukweli kuwa katika sheria nyingi za nchi za Kiafrika, ardhi "ni mali ya Serikali." Pia anatuonyesha mikakati muhimu na changamoto zilizopo katika kujenga vuguvugu imara la mabadiliko. Nasako Besingi anasema, “Ili vuguvugu la upinzani liweze kufanikiwa—ni muhimu sana kuimarisha mshikamano wa wananchi na kupata safari za mafunzo za kubadilishana uzoefu kati ya vijiji ambavyo vimeathiriwa moja kwa moja na vile ambavyo havijaathiriwa moja kwa moja na miradi mbalimbali ya uwekezaji—ili kuwajengea wananchi ujasiri katika ngazi za wananchi."

Kutoka Afrika Kusini, kuna makala inayotueleza juu ya Baraza la Kudumu la Watu, ambapo zaidi ya kesi ishirini toka katika eneo hilo ziliweza kuwasilishwa na kusikilizwa. Baraza limekuwa ni Jukwaa muhimu sana kwa wanajamii kuweza kuelezea mapambano yao na katika kujenga mshikamano. Kesi ya wananchi wa Xolobeni nchini Afrika ya Kusini imekuwa ni ishara bora. Mwezi Novemba 2018, baada ya miaka 16 ya mapambano dhidi ya kampuni kubwa ya uchimbaji wa madini ya Australia, mahakama iliamua kwa kuwapendelea wananchi; mahakama ikasema kuwa kabla ya kutoa kibali cha kumiliki na kuchimba madini ni lazima ridhaa “kamili na rasmi” itolewe na mji wa Xolobeni.

Makala nyingine inaelezea juu ya habari ya kampuni ya upandaji miti inayoitwa Green Resources nchini Tanzania. Makala hii inatuonyesha kuwa mara zote makampuni haya yanahitaji kupata eneo kubwa la ardhi, na ili yaweze kufanya hivyo, wao hutoa orodha ya ahadi nyingi ambazo mara nyingi huwa hazitekelezwi kwa lengo la kuwashawishi wanajamii ili waweze kuitoa ardhi yao. Hata hivyo, wananchi wa kijiji cha Nzivi walijifunza na kupata uzoefu kwa wakati na hivyo wakaamua kusema hapana kwa kampuni yoyote inayotaka kumiliki kiwango kikubwa cha ardhi yao. Makala hii inaonyesha umuhimu wa kupashana habari na hadithi mbalimbali kati ya wananchi wanaokabiliana na hali zinazo shabihiana.

Mapambano Bado Yanaendelea!