(Swahili) Upinzani wa Wanawake Walinzi wa Maeneo kwa Tasnia ya Uziduaji huko Amerika ya Kusini

Huko Amerika ya Kusini, wanawake wamekuwa ni sehemu ya historia ya mapambano katika harakati za kulinda maeneo yao na mazingira. Kwa kupitia maandamano yaliyoratibiwa na vitendo vingine vya kila siku, wanawake hao wameweza kuzuia namna mbalimbali za uziduaji na aina mbalimbali za vurugu dhidi ya wanawake. Pia wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano kama hayo, huku “wakitumia miili yao” kuzuia uharibifu wa maeneo yao, pia wametoa mawazo muhimu kuhusu mfumo-dume na hali ya ubaguzi iliyomo katika tasnia ya uziduaji. Kwa kutumia mkazo na tamko la wanawake kuwa “nafsi binafsi ni ya kisiasa” wameweza kuhoji vitendo vya ngono katika mavuguvugu ya kijamii, ukandamizaji wa kijinsia na majukumu ya kijinsia, na wameweza kutengeneza nafasi yao inayojitegemea kwa misingi ya mshikamano na hali ya kujaliana kwa pamoja. Katika makala inayofuata tutawashirikisha kuhusu tafakari kadhaa kuhusiana na mapambano ya wanawake hao, na tutatoa kwa ufupi juu ya hali ilivyo hivi sasa kuhusu mfumo wa tasnia ya uziduaji katika eneo hilo na madhara yake ya kipekee kwa maisha ya wanawake.

Tasnia ya uziduaji ni mfumo wa kiuchumi na kisiasa ambao misingi yake ni katika uundaji bidhaa na unyonyaji wa rasilimali usio zuiwa. Huko Amerika ya Kusini tasnia hii imeenea sana tangu miaka ya 1990. Tasnia hii ya uziduaji inaleta uharibifu ambao ni mgumu sana kuurekebisha kwa kuwa inachafua hewa, ardhi, na vyanzo vya maji na inasababisha upoteaji mkubwa wa bayo-anuai. Zaidi ya yote, tasnia hii inaingilia na kugongana na haki za pamoja za wanajamii, inaharibu mbinu mbalimbali za kiasilia za kimaisha na za kiuchumi za wanajamii, na hatimaye inawafanya wanajamii hao kuwa tegemezi wa masoko ya nje.

Tasnia ya uziduaji, katika namna zake mbalimbali, imegubikwa na uporaji na matumizi ya mabavu kinyume na sheria. Tasnia hii ina msingi wake katika ubaguzi ulio ndani ya mfumo na unaojidhihirisha kupitia unyang’anyaji wa maeneo ya watu ya kiasili, pia unaojidhihirisha kupitia tabia yao ya kukana maisha ya kidesturi ikiwemo namna ambazo makabila ya kiasili, wazawa wa kiafrika, na wanajamii wa visiwani waliochanganya asili zao (Raizales) wanavyofanya katika kulinda mazingira.

Jinsi gani tasnia ya uziduaji inavyofanya kazi Amerika ya Kusini?

Huko Amerika ya Kusini na maeneo ya Karibeani, tasnia hii ya uziduaji imejikita katika uporaji na vurugu ambapo madhara yake hasi na mabaya yanaonekana bayana, pia tasnia hiyo imegubikwa na mikakati mibaya inayofanywa na makampuni katika kunyang’anya ardhi na maeneo mengine kwa ushirikiano na serikali mbalimbali katika nchi ambazo shughuli hizo zinafanyika, na mara nyingi mambo hayo yanafanyika kwa ushirikiano na serikali za nchi ambako kampuni husika inatoka.

Ushirikiano wenye hila kati ya makampuni, serikali mbalimbali, na katika mazingira fulani uhusishwaji wa makundi haramu yenye silaha na mabavu mengine yanayofichwa, ni vitu vinavyoweza kuonekana sana katika hatua mbalimbali zinazohusisha migogoro mbalimbali ya kijamii na kimazingira kama ifuatavyo: a) sheria na sera zinazo wapendelea wawekezaji na makampuni katika nchi zinazolengwa; b) ukiukwaji wa haki ya kuwa na majadiliano ya kabla, yasiyo na masharti, na yenye taarifa za mapema na ushiriki wa asasi za kiraia, hali ambayo inaruhusu miradi kuanzishwa hata kama kuna upinzani wa wanajamii; c) ulinzi wanaopewa makampuni na vifaa vyao kwa kupitia uwekaji wa vifaa vya kijeshi katika maeneo huku ulinzi huo ukisimamiwa na makundi yenye silaha na uhalifu unaoratibiwa; na d) uingiliaji wa majaji, mahakimu, na waendesha mashtaka wanaokana kuwa makampuni hayo hayahusiki, na hivyo kusababisha hali ya kutojali kuadhibiwa kuendelea kuwepo.

Kwa sasa, Amerika ya Kusini inaendelea kuwa moja ya eneo lenye hatari sana kwa wale wanaojaribu kulinda maeneo yao: Asilimia 60% ya mauaji ya watu wanaolinda ardhi na mazingira katika maeneo yao duniani yamerekodiwa kufanyika katika eneo hili. Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni iliyochapishwa na asasi ya kimataifa ya ushuhuda inayojulikama kama (International NGO Global Witness) nchi ambazo zina kiwango cha juu cha mauaji hayo kipo katika nchi za Brazili, Kolombia, Honduras, Guatemala, Peru na Nicaragua. (2)

Moja ya mkakati unaotumiwa na makampuni na serikali katika kuzimisha upinzani ni kuwabambikizia watu mashtaka ya jinai, jambo hili linafanyika sana katika miradi yote mikubwa ya uziduaji. Jambo hili linatokea kwa kuwanyanyapaa wapinzani, kuwaharibia sifa katika vyombo vya habari au kupitia matamko ya maofisa wa serikali, ukandamizaji wa maandamano ya kijamii na matumizi ya madai ya kisheria au mashtaka ya jinai kwa watetezi wa wanajamii na mazingira. Hali hii inathibitisha uwepo wa mfumo wa sheria wenye upendeleo na usio zingatia haki na usawa kwa wote: wakati makampuni yanapofurahia usalama wa kisheria na ulinzi wa silaha katika harakati zao za kuyachukua maeneo yote, wale wanaopambana kuyalinda na kuyatetea maeneo yao wanateswa na kupewa vifungo vibaya kwa uonevu.

Ni jinsi gani wanawake wanaathirika kipekee?

Tasnia ya uziduaji imejikita katika kuendeleza mfumo dume, mfumo ambao una athari za kipekee kwa njia mbalimbali za kimaisha kwa wanawake. Kama ambavyo baadhi ya wataalamu wa kike na watetezi wa ardhi wanavyodai, kuna uhusiano wa kidesturi, kihistoria, na mifano mbalimbali inayoenda sambamba kati ya unyonyaji na hali ya kuitawala miili ya wanawake na mazingira ya kiasili. Kwa mfano, katika muktadha wa uchimbaji madini na uchimbaji wa mafuta na uwekezaji wa mabwawa ya maji ya kuzalishia umeme, hali ya ‘kudumisha mfumo-dume’ katika kumiliki na kutawala maeneo na ardhi kunafanyika kwa makusudi (3) ambapo nafasi ya jamii na maisha ya kila siku yanabadilishwa ili kukidhi matakwa na mahitaji ya kundi moja la kijinsia la wanaume lenye mfumo-dume.

Watetezi wa haki za ardhi na wanawake wanathibitisha kuwa vitendo vya kutoweka kwa ardhi na uchafuzi wa maeneo vinatokea huku vikiandamana na kurudi kwa vurugu za wanaume dhidi ya wanawake na wasichana ikiwemo kuongezeka kwa ukosefu wa usawa wa kijinsia. Mambo hayo yanatokea katika maeneo yote ya maisha yao na yanaweza kuthibitishwa kutokana na uwepo wa mambo yafuatayo: a) ongezeko la mzigo wa kazi kwa maana ya majukumu yanayofanywa na wanawake; b) kupotea kwa uwezo na uhuru wa kiuchumi na usalama wa chakula; c) kuongezeka kwa vurugu za kisaikolojia, kimwili, kiuchumi, mfumo-dume na vurugu za kingono katika muktadha wa familia na jamii; d) ongezeko la athari mbaya za kimwili, kihisia na katika afya ya uzazi kutokana na uchafuzi wa hewa, ardhi na maji; e) ubaguzi kwa msingi wa kijinsia na ukiukwaji wa haki za ushiriki wa wananchi kwa msingi wa kanuni inayozingatia mchakato wa ushirikishwaji wa kabla, pasipo masharti, na wenye taarifa za mapema (4); f) kuongezeka kwa unyonyaji wa kingono kwa wanawake na wasichana na; g) kupotea kwa utambulisho wa kiutamaduni na kudhoofika kwa majukumu ya kiasili ya wanawake katika jamii.

Vurugu dhidi ya wanawake walinzi wa maeneo

Hatari maalum na ambayo imekuwa ikiwakumba wanawake walinzi wa maeneo mara kwa mara ni nyongeza tu ya madhira ambayo wanawake wamekuwa wakikabiliana nayo kihistoria, mateso hayo yanatokea kutokana na uwepo wa mfumo wa kijamii ambao umegubikwa na kutokuwepo kwa haki na udhalimu wa kijinsia, ubaguzi, na matabaka. Kinyume na ilivyo kwa wanaume, walinzi wanawake wanakabiliana na vurugu za aina mbalimbali, hasahasa unyanyasaji wa kingono. Pamoja na kupata mashambulio toka kwa makampuni na mawakala wa serikali, walinzi hao wa kike wa maeneo wanakabiliana na vurugu mbalimbali kila siku katika muktadha wa familia na jamii zao, na mara nyingine wanakabiliana na vurugu hata katika mashirika yao na mavuguvugu mengine ya kijamii.

Ingawa takwimu za wanawake waliouawa ni ndogo ukilinganisha na zile za ndugu zao wanaume, ni muhimu kuuangazia uhalisia uliopo katika uchunguzaji wa kesi za “mauaji ya wanawake wanaolinda maeneo yao” kama wanawake walinzi wa maeneo wa Guatemala wanavyouita uuaji huo "Kwa Kiingereza: territorial femicides," (6) ni dhahiri kuwa uchunguzi wa mauaji ya wanawake unashughulikiwa tofauti na ule wa wanaume. Kutokuwepo kwa utambuzi wa kazi ya wanawake watetezi na upendeleo wa mamlaka za kisheria wanaotumia chuki dhidi ya wanawake na upendeleo wa kibaguzi unasababisha kesi zao nyingi kuchukuliwa kuwa ni “uhalifu unaotokana na wivu wa kimapenzi,” na hivyo kudharau muktadha wa upinzani unao ongozwa na wanawake kama hao na wakati mwingine hata kubuni na kutunga kuwa kesi za jinsi hiyo ni za kujiua na kujitoa mhanga, jambo ambalo kimsingi linasabibisha na kuimarisha hali ya kutojali na kutoogopa kuchukuliwa hatua. (7)

Kwa sababu hiyo, vurugu za jinsi hiyo haziishi kwa kuuondoa uwepo wa kimwili wa wanawake watetezi: namna ambavyo uchunguzi unafanyika, au kwa lugha nyingine kuwafanya wanawake waonekane waovu, na kuwageuza ili wawe watu wabaya, na kuzuia haki na malipo kwa wanawake hao na familia zao hakusaidii chochote katika kumaliza vurugu dhidi ya wanawake.

Pia vurugu tofauti zimesababisha uwepo wa madhara tofauti katika maisha ya wanawake watetezi. Athari hizo mbaya ni pamoja na za kimwili, kihisia na kuathirika kwa afya ya kiroho, madhara ambayo huonekana kupitia hali ya kukosa usingizi, kupungua uzito, kujawa na hofu ya kudumu, msongo wa mawazo, na hata baadhi ya magonjwa hatarishi kama vile kansa. Pia matendo ya kubambikiziwa makosa ya jinai na kunyanyapaliwa yamekuwa na athari zilizo wazi katika shughuli zao za kiuchumi, na mara nyingi wamekuwa wakitengwa hata katika jamii na familia zao. Katika ngazi ya pamoja, vurugu hizi zinayadhoofisha mashirika yao, zinaleta hofu miongoni mwa wanawake na wakati mwingine zinasababisha mpasuko au mkwamo katika mapambano yao.

Mapendekezo toka kwa wanawake wa Amerika ya Kusini kwa ajili ya kuyalinda maeneo yao na kuondoa vurugu dhidi ya wanawake

Katika mfumo wa kazi yao kama watetezi na watunzaji wa mazingira na hali ya asili, wanawake wamejiundia matendo fulani ambayo yamesaidia katika kutoa msimamo na mitazamo yao juu ya madai kadhaa, na katika nyakati nyingi wanawake hao wameweza kuzuia au kusimamisha shughuli kadhaa za uziduaji ambazo zinatishia maeneo yao. Pia, wameweza kuzalisha mabadiliko muhimu sana katika ngazi binafsi na pia katika ngazi ya pamoja, wameweza kufanya hivyo kwa kutengeneza vitendo ambavyo vinalenga kuimarisha ulinzi na usalama madhubuti.

Moja kati ya hazina zao za vitendo vya kijamii ni pamoja na: a) kutengeneza nafasi kwa ajili ya mijadala na kubadilishana uzoefu wa namna ya kujilinda katika ngazi ya kitaifa na kikanda na katika kujenga mitandao ya kikanda ili kuimarisha hali ya kuonekana na kujulikana, kupata washirika, na kujenga vitovu vya upinzani katika ngazi ya chini ya jamii; b) kuandamana na vitendo vya upinzani vya moja kwa moja bila kupingwa ili kuzuia kusonga mbele kwa shughuli za uziduaji, na kuirejesha ardhi iliyoporwa: yaani matendo kama kufunga barabara, maandamano, kambi za kudumu ili kuzuia ufungaji mitambo ya kampuni; c) vitendo vya nguvu za kisheria ili kuamsha namna mbalimbali za ulinzi katika mfumo wa kitaifa na kimataifa, na pia shughuli za utetezi zinazolenga kuwafikia viongozi wa serikali za mitaa na mamlaka za kitaifa, na kuyafikia pia mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu; d) kuandika ripoti zinazohusu vitendo vya vurugu na ubambikiziaji kesi kwa walinzi wa kike, na pia uundaji mikakati ya mawasiliano ili kuyafanya mapambano yao yaweze kusikika; e) kuhamasisha majadiliano huru na binafsi ili wanajamii waweze kuelezea nia na mawazo yao kuhusu maamuzi na vitendo vinavyoathiri mazingira yao, na haja ya kuwa na majadiliano ya kabla ya mradi kwa mujibu wa viwango vya kimataifa; f) vitendo vya kila siku vya upinzani kwa lengo la kulinda usalama wa chakula – kupitia uhifadhi wa mbegu za asili na matumizi yake ya kiasili, vitendo vya kilimohai vinavyohifadhi ikolojia – ikiwemo njia mashuhuri inayojulikana kama uchumi wa kike wa mshikamano na g) vitendo na tafakari kuhusu namna ya kujilinda binafsi na namna ya kujilinda kwa pamoja, ikiwemo jitihada za uponyaji binafsi na uponyaji wa pamoja.

Moja kati ya michango mikuu ya mapambano ya wanawake na watetezi wa nadharia ya haki na usawa wa wanawake kwa ajili ya ulinzi wa ardhi na maslahi ya pamoja ni ule wa kukazia uhusiano uliopo kati ya miili na maeneo ya kuishi. Watetezi wa wanawake wa Guatemala wameshauri uwepo wa hoja inayohusu mwili-ardhi na eneo katika kuyaangazia mapambano ya kulinda ardhi dhidi ya tasnia ya uziduaji, hoja imejikita kuwa mambo hayo mawili ni lazima yaende pamoja bila kutenganishwa katika mapambano ya wanawake katika maeneo hayo ili waweze kuishi maisha ya huru mbali na vurugu na unyonyaji wa miili yao.

Kutokana na uzoefu wao kama watetezi wa ardhi, wanawake wameweza kulazimisha uwepo wa nafasi ya mabadiliko kwa msingi wa utunzaji na uangalizi wa uhai katika namna zake zote, ikiwemo jitihada jumuishi zinazo ongezeka katika kuitunza dunia na kujitunza wao wenyewe kwa ujumla, na mambo hayo ni muhimu sana katika uanaharakati wao. Maono haya mapana ya utunzaji na uangalizi yanaonekana kwa namna ambavyo baadhi ya mashirika ya wanawake na yale ya makabila ya kiasili yanavyo itazama dhana nzima ya ulinzi: ulinzi wa watetezi wa haki za wanawake na watetezi wa mazingira ni muhimu sana na mambo hayo yamefungamana na ulinzi wa ardhi na maeneo. Kwa fikra hii, mashirika yanapendekeza hatua za ulinzi na vitendo vinavyojumuisha masuala ya kiroho ya makabila ya kiasili, wazawa wa kiafrika na jamii zilizochanganyikana za visiwani (Raizales). Katika muktadha huu, uponyaji unakuwa ni jambo muhimu sana: kutokana na mjadala wenye ufahamu tofauti kati ya watu mbalimbali, mazingira na vizazi tofauti, na kutokana na hatua ya kuzirejelea kumbukumbu za wahenga, walinzi wa wanawake sio tu kwamba wanaleta uponyaji kutokana na athari mbaya za uvamizi walioteseka nao kutokana na uanaharakati wao wa mazingira, bali pia wanaponya majeraha makubwa ya kimfumo ya vurugu dhidi ya wanawake.

Laura María Carvajal Echeverry, ni Mratibu wa Program ya Wanawake na Maeneo iliyo chini ya Mfuko wa Hatua za Haraka (Kwa Kiingereza: Urgent Action Fund) kwa ajili ya Amerika ya Kusini na Karibeani (8)

(1) Makala hii inatokana na chapisho letu linaloitwa “Tasnia ya Uziduaji Amerika ya Kusini. Athari kwa Maisha ya Wanawake na Mikakati ya Kulinda Maeneo – Kwa kiingereza: Extractivism in Latin America. Impacts on women's lives and strategies for the defense of territory," linalopatikana katika tovuti yetu kwa anuani hii: https://www.urgentactionfund-latinamerica.org/site/assets/files/1346/b81245_6cc6d3d7edd447d0ab461860ae1ae64f.pdf

(2) GLOBAL WITNESS, 2018. At what cost? Irresponsible business and the murder of land and environmental defenders in 2017. Available at: https://www.globalwitness.org/en/campaigns/environmental-activists/at-what-cost/

(3) See: CABNAL, Lorena. Without being consulted: the commodification of our body-land territory, in: Women Defending the Territory. Experiences of participation in Latin America. Urgent Action Fund of Latin America and the Caribbean, 2015, https://issuu.com/fondodeaccionurgente-al/docs/territorio_engl; and GARCÍA TORRES, Miriam. Feminism reactivates the struggle against 'extractivism' in Latin America. Published in La Marea on 17 February 2014, by the Latin American Network of Women Defenders of Social and Environmental Rights;, https://www.rebelion.org/noticias/2014/2/181047.pdf (Andiko hili linapatikana kwa Kihispania tu)

(4) Kwa mitazamo mipana kuhusu ushiriki mkamilifu wa wanawake katika masuala ya mazingira na kuhusu uzoefu wa wanawake katika nchi mbalimbali kwa msingi wa dhana ya uhuru wa majadiliano ya kijamii, tunaomba uangalie machapisho yetu ya pamoja na wanawake walinzi kutoka Argentina, Guatemala, Bolivia na Ecuador: Women defending the territory: experiences of participation in Latin America | 2015, chapisho linapatikana hapa kwa lugha ya kiingereza: https://issuu.com/fondodeaccionurgente-al/docs/territorio_engl

(5) Kwa mtazamo wa kina kuhusu ubambikiziaji wa kesi za jinai na mashambulizi dhidi ya wanawake walinzi wa maeneo, tazama Ripoti yetu ya Kikanda Kuhusu Aina za Jinai na Vikwazo vya ushiriki mkamilifu wa wanawake wanaolinda haki za mazingira, maeneo na uoto wa asili katika bara la Amerika inayopatikana hapa: https://fondoaccionurgente.org.co/site/assets/files/1348/ingles.pdf

(6) Aina hii ya uelewa imekuwa ikihamasishwa na wanawake walinzi wa maeneo, wakiwemo Red de Sanadoras del Feminismo Comunitario de Guatemala (Network of Healers of Community Feminism of Guatemala).

(7) Kwa mapitio na mtazamo mpana wa hali ya kutojali na bila kuogopa kuadhibiwa, tazama Ripoti yetu ya Kikanda Kuhusu Kutojali Vurugu dhidi ya Wanawake Walinzi wa Maeneo, Bidhaa za Pamoja, na Uoto wa Asili katika Amerika ya Kusini, 2018, inayopatikana hapa: https://www.urgentactionfund-latinamerica.org/site/assets/files/1343/regional_report_-_impunity.pdf

(8) Mfuko wa Haraka wa Amerika Kusini na Karibeani inayoongea Kihispania ni mfuko wa kikanda wa kike unaochangia kuleta uendelevu na kuwaimarisha wanaharakati na mavuguvugu yao, kwa lengo la kimkakati kwa kuzingatia hatari na fursa. Tunaunga mkono upinzani, mapambano na madai ya wanawake walinzi wa haki na maeneo katika harakati za kubadili mfumo usio na haki na usawa, kwa kusisitizia juu ya ulinzi wa wanawake watetezi: https://fondoaccionurgente.org.co/en/