(Swahili) Tafakari kutoka Afrika: Ishinde hofu ya kujenga vuguvugu imara la mabadiliko

Sekretarieti ya shirika la WRM International ilifanya mahojiano na mwanaharakati wa masuala ya kijamii na kimazingira na mtetezi wa haki za binadamu Ndugu Nasako Besingi. Yeye ni Mkurugenzi wa shirika la Kikameruni linaloitwa Struggle to Economize the Future Environment (SEFE) – (Kwa Kiswahili: Mapambano ya Kuyalinda Mazingira ya Baadaye), shirika hili linazisaidia jamii za vijijini katika mapambano yao ya kupata haki zao za ardhi dhidi ya makampuni ya mashamba makubwa ya michikichi ya mawese. Ndugu Nasako aliwaandaa wanajamii kuandamana na kupinga uendelezaji wa mashamba ya michikichi ya mawese kunakofanywa na kampuni ya kimarekani ya Herakles Farm. Kutokana na harakati hii, alijikuta akiwa ni mhanga wa kampuni ya Herakles Farm na akawa pia mhanga wa serikali akikabiliana na manyanyaso ya kushambuliwa kimwili, kutishiwa, na kubambikiziwa kesi za uhalifu. Mwanaharakati huyu alikemea na amekemea vikali ukiukwaji wa haki za binadamu katika ukanda unaozungumza lugha ya kifaransa nchini Kameruni.

Mara nyingi, utasikia maelezo kuwa jamii za Afrika haziwezi kuzilinda wala kuzidai ardhi zao toka kwa makampuni ambayo yamepata hati za kukodishiwa ardhi toka kwenye serikali za kitaifa, kwa kisingizio kuwa Sheria za kitaifa zinadai kuwa, “ardhi yote ni mali ya Serikali”. Wewe una mtazamo gani katika hoja hii?

Jambo la kwanza la kutafakari ni hili, ni kitu gani kinachounda Serikali? Serikali ni lazima iwe na mambo makuu manne yafuatayo: watu, eneo la utawala, dola, na utawala. Hivyo sentensi inayosema kuwa, “ardhi yote ni mali ya Serikali” haimaanishi kuwa ardhi yote inamilikiwa na serikali, bali ina maanisha kuwa ardhi yote inamilikiwa na watu wote wanaoishi katika himaya ya Serikali husika, wakiwemo watu waliopo ndani ya serikali. Sehemu kubwa ya watu katika Serikali nyingi ni wale wanaoishi katika maeneo ya wananchi vijijini, ambapo kila siku wanapambana kuzilinda ardhi zao na maeneo wanayoishi. Kwa upande mwingine, serikali inaweza kuelezewa vizuri kuwa ni wakala ambaye ndiye msimamizi na ambaye DHAMIRA ya Serikali imeundwa juu yake, inatekelezwa, na kusimamiwa kupitia sera za pamoja ambazo zinafafanua juu ya mwelekeo na maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii. Ukiyatafsiri majukumu hayo hayaleti maana kuwa haki zote zipo juu ya serikali kuhusu ardhi pamoja na rasilimali zilizomo ndani ya Serikali.

i makosa kwa serikali yoyote ile kudai kuwa inamiliki ardhi, huku ikizitupilia mbali haki za wananchi kumiliki ardhi. Kwa hakika, tatizo lililopo katika sheria nyingi za ardhi barani Afrika zinatokana na ukweli kuwa ziliandikwa kwa usaidizi wa watawala wa kikoloni, ambao pasipo hata ridhaa ya wananchi, waliyakabidhi maeneo na himaya zote kwa maraisi, huku wengi wao wakiwa ni wale ambao hawakuchaguliwa na wananchi, yaani waliteuliwa tu na wakoloni ili kulinda maslahi ya wakoloni ya muda mrefu. Zaidi ya yote, dhana inayoeleza kuwa “ardhi yote ni mali ya Serikali” haiipatii serikali haki ya kumiliki ardhi na kisha kuitumia kadri itakavyo, bali inaipatia serikali haki ya kuisimamia na kusajili masuala yote yanayohusu ardhi huku ikizingatia na kuheshimu maslahi ya wanajamii.

Ni jukumu la serikali zote kuhakikisha kuwa wananchi wake wanakuwa na furaha, uhuru na amani na pia ni sharti serikali ilinde mali na amana za watu. Kwa nyongeza, serikali hizi zimesaini na kukubaliana na mikataba ya kimataifa kwa niaba ya Serikali za watu ili kulinda haki za wananchi. Kwa kuwa sheria za kimataifa ziko juu kuliko sheria za kitaifa, itakuwa ni sahihi kueleza kuwa kitendo cha kusaini na kukubaliana na miongozo ya kimataifa kunazishinda nia za serikali kugawa ardhi kwa kutafsiri vibaya kifungu kinachosema “ardhi yote ni mali ya Serikali”, pasipo ridhaa toka kwa watu, ambao maisha yao ya kila siku yanategemea sana ardhi zao.

Azimio la Kimataifa kuhusu Haki za Binadamu, ambalo linapatikana katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa, Mkataba wa Afrika kuhusu Watu na Haki zao, na mikataba mingine ya kimataifa linaharamisha vitendo vya serikali kuchukua ardhi kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo pasipo kupata ridhaa toka kwa wananchi. Hivi karibuni, Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia Uhalifu wa Kivita ilikuwa inatafakari juu ya uporaji wa ardhi na ukiukwaji wa haki za wananchi kama moja ya uhalifu unaopaswa kuangaliwa na kushughulikiwa katika ngazi ya kimataifa na ikaahidi kuwachukulia hatua wale wote wanaokiuka haki hizo za wananchi (kwa maana ya serikali mbalimbali na makampuni).

Tangu nilipoanza kujishughulisha na masuala ya haki za wananchi kuhusu ardhi kupitia mashirika mbalimbali na vuguvugu la mabadiliko nchini Kameruni na nchi zingine, sijawahi kukutana na jamii hata moja inayokubaliana na wazo au dhana kuwa ardhi inamilikiwa na serikali. Jamii nyingi zilieleza dhahiri na waziwazi kuwa ardhi ni mali ya jamii na urithi toka kwa wahenga wao. Hakuna hata jamii moja niliyofanya nayo kazi inayokubaliana na uwepo wa makampuni ya kimataifa katika ardhi zao, wananchi wanadai kuwa makampuni hayo yalianzishwa kwa mbinu za mabavu.

Kwa uzoefu wako, ni mambo gani muhimu/ama ni mikakati gani mizuri katika kujenga vuguvugu la mabadiliko na kuimarisha mapambano ya wananchi kwa kuzingatia muktadha wa Kiafrika?

Vuguvugu la mabadiliko na mapambano ya wananchi barani Afrika bado yapo katika hatua za awali kutokana na historia ya Afrika iliyogubikwa na giza la utumwa, ukoloni, ukoloni mambo leo uliojitokeza mara baada ya uhuru, huku kukiwa hakuna fursa za kidemokrasia na haki za binadamu. Leo hii hali inaonekana kuwa tofauti sana, huku kukiwa na demokrasia kwa kiasi fulani na matumizi kidogo ya haki za binadamu kunako shinikizwa na nchi zilizoendelea kiviwanda.

Jambo muhimu zaidi katika kujenga vuguvugu imara la mabadiliko barani Afrika ni kuishinda hofu na ujinga ulioingizwa kwa makusudi na utawala wa wakoloni na utawala wa kikoloni-mamboleo uliofuata baada ya ukoloni. Jambo jingine muhimu la kuzingatia ni kuainisha mahitaji ya jamii huku kukiwa na jitihada za makusudi za kukuza uelewa na miongozo yenye kutoa elimu kuhusiana na mahitaji hayo ya wananchi. Jambo jingine muhimu ni kuimarisha uwezo wa wanaharakati na watetezi wa wananchi na asasi za kiraia ili waweze kufahamu haki zao na namna ya kuzilinda kwa kuzingatia shughuli zao mbalimbali za kila siku za kimaisha. Ukweli ni kuwa vuguvugu la mabadiliko imara na la kudumu ni lile linalojengwa kutoka ndani na si nje, hii ina maanisha kuwa vuguvugu imara la mabadiliko ni lazime litokee ikiwa limezingatia changamoto za wananchi.

Baadhi ya mikakati ya kuweza kusonga mbele ni pamoja na: kuanzisha jumuiko imara la kiafrika la asasi za kiraia na wananchi barani Afrika kwa lengo la kupashana habari na uzoefu; kupanga na kutekeleza shughuli mbalimbali katika maeneo ya wananchi kuhusu haki za ardhi; kusaidia shughuli za ushawishi na uchechemuzi katika kulinda na kutatua vurugu na ukiukwaji; kusaidia uwepo wa aina mbalimbali za vitu vinavyotoa elimu kwa wananchi; na hatua nyingine ni kutengeneza miongozo na video mbalimbali za taarifa katika lugha rahisi zinazoeleza na kufafanua mikakati na mbinu mbalimbali inayotumiwa na makampuni katika kujipenyeza na kuzifikia jamii na kisha kuzipora ardhi za wahenga wao.

Je, changamoto kuu ni zipi?

Katika muktadha wa Afrika, kuna changamoto nyingi sana ambazo zinahitaji mbinu tofauti ili vuguvugu la mabadiliko liweze kufanikiwa. Changamoto ya msingi sana hapa ni ujinga na hali ya wananchi wengi kutokuwa na ufahamu kuhusu haki za ardhi na jinsi ya kuzilinda ardhi za wahenga wao, na hii inatokana na kutokuwa na uwezo wa kupambana na kuzuia nguvu inayokuja kwao ikiwa na nia ya siri ya kunyang’anya ardhi zao kunakofanywa na makampuni na serikali mbalimbali. Changamoto nyingine ni uongozi mbaya uliogubikwa na rushwa na umaskini kwa lengo la kuwafanya wananchi kuyanyenyekea mapenzi ya serikali. Pia kuna vikwazo vya kisiasa ambavyo vinawekwa na serikali ili kuminya haki za NGOs, asasi za kiraia (AZAKI), pamoja na mavuguvugu mengine ya mabadiliko ya kijamii, kupitia vitisho na kubambikiziwa kesi za uhalifu. Pia mitandao inayoendesha vuguvugu la mabadiliko ni lazima iwe tayari kukabiliana na mazingira magumu na ukosefu wa fursa za rasilimali fedha.

Kwa mtazamo wako, unafikiri mshikamano wa kimataifa ni muhimu katika kusaidia mapambano ya wananchi?

Mshikamano wa kimataifa ni jambo pekee bora lililobakia ili kuweza kuzuia uporaji wa kijinga wa ardhi ya wananchi. Jambo hili ni la muhimu sana ili kuweza kumaliza ushirikiano wenye kificho kati ya makampuni na serikali mbalimbali kwa kutumia ujinga wa wananchi, kuwanyonya wananchi na hatimaye kupora ardhi zao.

Hatua ya kwanza muhimu ni upatikanaji wa elimu na ufahamu kuhusu haki ambako kutasababisha uwepo wa vuguvugu imara la kudai mabadiliko na kupinga wizi na uporaji wa ardhi. Kutoa elimu kupitia upashanaji habari katika ngazi ya chini ya wananchi, ambako ndiko ukiukwaji mkubwa unafanyika, na kisha kutoa taarifa za ukiukwaji katika zile nchi zinazotoa fedha kwa makampuni na nchi nyingine waliko wateja wa bidhaa zao.

Vikundi vya ngazi ya chini vinaweza visiwe na uwezo wa kuvishinda vitisho peke yao, vurugu na ukiukwaji, ikiwemo mlolongo wa kuzitupilia mbali na kuzikanyaga kesi za kisheria zinazolenga kuwashtaki serikali na makampuni. Mara nyingi vikundi hivi havina uzoefu wa kutosha wa kutumia mbinu zisizohusisha vurugu ambazo zinajumuisha mambo kama kuwa na ufahamu sahihi na akili ya kukabiliana na wale wanaokiuka na waonezi.

Ni aina gani ya mshikamano wa kimataifa unaofikiri umefanya vizuri hadi sasa?

Hadi sasa, na katika muktadha wa Kiafrika, ninaweza kuifikiria kampeni moja nchini Kameruni dhidi ya kampuni ya Herakles Farms, ambayo ni kampuni ya kimarekani ambayo ilikuwa imeazimia kukata na kusafisha hekta 73,000 za misitu ya asili safi kabisa ili iweze kuanzisha mradi wake wa mashamba ya michikichi ya mawese katikati ya maeneo manne yaliyohifadhiwa, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Korup. Vuguvugu ka kuipinga kampuni ya Herakles Farms lilitoka kwa wananchi, asasi za kitaifa na kimataifa, watafiti, wanasayansi, wanazuoni, na wengine wengi. Hivyo kukawa na shinikizo la juu sana kwa wakati mmoja, yaani kutoka ngazi za chini mahali ambapo kampuni hiyo ilikuwa ikifanya kazi, na pia kukawa na shinikizo la juu toka katika ngazi ya kimataifa, ambako kampuni ilikuwa ikitafuta fedha kwa ajili ya kuanzishia na kugharamia mradi huo. Mwaka 2013, raisi wa Kameruni alisaini mfululizo wa amri ili kupunguza kiwango cha ardhi ambacho mtu au kampuni inaweza kupangishiwa kutoka hekta 73,000 hadi hekta 19,843. Lakini jambo hili bado halikuwapendeza wanajamii wengi na wakawa na nia ya kuendelea kupinga na kusimamia hoja yao ya awali kuwa “Hakuna Mashamba Makubwa Katika Ardhi Yetu”. Mwaka 2015 kampuni hiyo iliyatelekeza mashamba yake na shughuli zake katika ardhi za maeneo ya Mundemba na Toko.

Hata hivyo, ushirikiano wa kimataifa kama ule uliohusisha mashirika ya GRAIN/WRM na asasi za kiraia katika ngazi za kitaifa na asasi za wanajamii barani Afrika chini ya usimamizi wa muungano unaohusika katika Kupinga Ukuaji wa Mashamba Makubwa ya Michikichi ya Mawese kwa Matumizi ya Viwanda katika Afrika ya Kati na Magharibi. (kwa kiingereza: “Alliance Against Industrial Oil Palm Expansion across central and west Africa), umefanya kazi ya maana sana ya kuwaamsha wananchi waliokuwa wanateseka kwa kuyafanya mapambano yao yaweze kuonekana, kwa kuwapa taarifa na kisha kwa pamoja kutambua fursa zinazoweza kutumika kuzuia mashamba makubwa ya michikichi ya mawese yanayoleta uharibifu kupitia programu za kijamii za kubadilishana uzoefu na mawazo, kama vile warsha mbalimbali na safari za kuvitembelea vijiji ili kuwatia moyo katika harakati za kupinga uporaji wa ardhi zao. Pamoja na hayo kazi hiyo ya pamoja ililenga kuianika mikakati na mbinu zinazotumiwa na makampuni ya kimataifa yanayopora ardhi za wananchi na kisha kuwatahadharisha wale ambao wapo katika hatari ya kukutana na uporaji huo.

Je, kuna aina nyingine ya mshikamano ambayo ungependa itumike katika kuimarisha upinzani dhidi ya uporaji wa ardhi nchini Kameruni na kwingineko barani Afrika?

Ili vuguvugu la upinzani liweze kufanikiwa, ni muhimu sana kuimarisha mshikamano wa wananchi na kupata safari za mafunzo za kubadilishana uzoefu kati ya vijiji ambavyo vimeathiriwa moja moja na vile ambavyo havijaathiriwa moja kwa moja na miradi mbalimbali ya uwekezaji ili kuwajengea wananchi ujasiri katika ngazi za wananchi. Mambo mengine ya muhimu ni: suala la kubadilishana uzoefu katika ngazi ya mabara ili kushirikishana uzoefu, mambo ambayo yanasaidia sana katika kuuanika uovu wa makampuni na mbinu zao; kuvitembelea vijiji ili kuvitahadharisha vijiji vilivyoathiriwa na ambavyo vinakaribia kuathiriwa juu ya upanuzi mbaya wa mashamba ya michikichi ya mawese na miradi mingine pasipo ridhaa yao; uanikaji imara wa udanganyifu unaofanywa na makampuni kuhusu maendeleo endelevu na jinsi wanavyogubikwa na fedha na makampuni mengine badala ya kuheshimu haki za wananchi kwa kuzingatia Ridhaa Inayozingatia Uhuru, na Taarifa za Awali (Kwa Kiingereza: Free, Prior and Informed Consent).

Tunatakiwa kufungamanisha upinzani wa wananchi wa chini pamoja na fursa za jumla za wananchi hao. Tunapaswa kuwekeza katika kujenga uwezo wa asasi za kiraia na wananchi wanaofanya kazi katika ngazi ya chini ili kuwa na “Upinzani wa Wananchi wa Kuaminika” unaoweza kuwaanika na kuwashinda nguvu waporaji wa ardhi na wakiukaji wa haki za binadamu katika bara ambapo kunakuwa na changamoto hizo. Kuandaa mfululizo wa matukio kama vile warsha, semina, safari za kutembelea vijiji, mikutano ya ana kwa ana na ile isiyo ya ana kwa ana na wahusika wakuu.

Kuna hitaji kuu la kujenga ushirikiano imara kati ya jamii na asasi za kaskazini na wenzao wa kusini ili kuweza kushughulikia tatizo la uporaji wa ardhi na uharibifu wa misitu, kwa kuwa mambo hayo yanaletwa na kutekelezwa na wawekezaji pamoja na sera za serikali ikiwemo ile ya chaguo la walaji katika nchi za kaskazini. Mikutano ya kubadilishana uzoefu kati ya wananchi wa Kaskazini na wale wa Kusini itawezesha uwepo wa ufahamu mzuri juu na namna maamuzi ya kisiasa, serikali mbalimbali na makampuni yanavyoleta athari kwa mazingira na ukiukaji wa haki za binadamu Kusini mwa dunia, hasa pale makampuni yanapotoa mawasiliano na matangazo yaliyojaa uongo kwa lengo la kuficha uharibifu na manyanyaso yao, huku wakizitangaza bidhaa zao kuwa ni endelevu.